Alhamisi, 21 Novemba 2013

DRC YASEMA UGANDA INA MASLAHI BINAFSI NA WAASI WA M23


Hatua ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kukataa kusaini mkataba wa amani na kundi la waasi la M23, imepeleka kilio kwa kundi hilo, na sasa wanashindwa kuelewa hatima yao nchini Uganda.

Uganda, nchi ambayo ni msuluhishi wa mgogoro huo baina ya DRC na waasi wa M23, imejikuta katika wakati mgumu kwani kundi la waasi wa M23 wapatao 1,700.

Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende, mwishoni mwa wiki ametamka kuwa “Serikali ya DRC ina wasiwasi kuwa Uganda ambayo kwa sasa inaonekana kuwa sehemu ya mgogoro na imeshindwa kuficha maslahi yake binafsi na waasi wa M23. Kwa sababu hiyo hatuko tayari kutia saini mkataba unaosimamiwa kwa mitego.”

Kauli hii ya Mende imekuja siku chache baada ya DRC kukataa kutiliana saini na waasi kwa maelezo kuwa M23 ni kundi lililotangaza kujivunja, wamekimbilia Rwanda na Uganda, na hivyo kulipa sharti kubwa wanalolikataa.



Sharti hilo ni kuwa mkataba uwe na kipengele kinachowazuia M23 milele kutoshika silaha na kuanzisha mapambano, hoja inayokataliwa na waasi, huku Uganda ikizishawishi pande mbili zitie saini mkataba hivyo hivyo ulivyo kwa maelezo kuwa yakitokea matatizo mbele ya safari utarekebishwa tena.


Masharti mengine wanayowapa waasi hao ni kuwa makamanda wapatao 100 waliokuwa wanaongoza kundi la M23, wasiruhusiwe kuingia jeshini moja kwa moja, na badala yake wapewe mafunzo ya kijeshi, huku wakiacha fursa ya kushitaki wahalifu wa kivita watakaothibitika mbele ya safari kuwa walitenda uhalifu dhidi ya binadamu.

Uganda pia imetishia kwa mara nyingine mwishoni mwa wiki kuwa ikiwa suluhu haitapatikana haraka, na DRC ikaendelea kuituhumu kuwa inashirikiana na waasi wa M23, basi yenyewe itajitoa katika nafasi ya kuwa msuluhishi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni