Rais Jakaya Kikwete ameiongezea tena muda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuiwezesha kumaliza kazi yake.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu juzi usiku, ilisema Rais Kikwete ameiongezea siku 14.
Tume hiyo ambayo ilitakiwa kumaliza kazi yake, Desemba 15, mwaka huu itaendelea na kazi kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 30, mwaka huu.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi yake. Baada ya maombi yake ya kwanza, Rais Kikwete aliiongezea Tume hiyo siku 45 kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu.
Kabla ya kuomba kuongezewa muda, ilitakiwa kukamilisha kazi yake kesho.
Rais Kikwete ameiongezea Tume hiyo muda zaidi kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza Tume hiyo kufanya kazi kwa miezi 18 licha ya kuwa sheria inampa Rais mamlaka ya kuiongezea tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku 60.
Kwa uamuzi wake, wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete atakuwa ameiongezea tume hiyo jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria.
Hatua hiyo ilitarajiwa hasa baada ya Tume hiyo kusimamisha kazi zake kwa muda baada ya kifo cha mmoja wa wajumbe wake, Dk Sengondo Mvungi kilichotokea Novemba 12, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa anatibiwa baada ya kujeruhiwa kwa mapanga na watu wasiojulikana nyumbani kwake Novemba 3, mwaka huu.
Baada ya kifo hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alitangaza kusitishwa kwa muda shughuli za Tume hiyo.
Kifo cha Dk Mvungi, ambaye aliteuliwa kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi kilikuwa pigo kwa Tume hiyo kwani mwanasheria huyo alikuwa amebobea katika masuala ya katiba.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotolewa Juni 4, mwaka huu.
Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania. Mh. Dr Jakaya Mrisho Kikwete. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni